AFRIKA KUSINI-ZIMBABWE

Mahakama kuu nchini Afrika Kusini yaagiza ofisi ya mwendesha mashtaka kuwachunguza maofisa wa Zimbabwe

Mmoja wa watu ambao wanaeleza kuteswa na polisi nchini Zimbabwe
Mmoja wa watu ambao wanaeleza kuteswa na polisi nchini Zimbabwe Reuters

Mahakama kuu nchini Afrika Kusini imeiagiza ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali kuwachunguza baadhi ya maofisa wa Serikali ya Zimbabwe ambao wanatuhumiwa kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji raia wa Zimbabwe waliokimbilia nchini humo. 

Matangazo ya kibiashara

Kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na viongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement Democratic Change ambao wamekimbilia nchini Afrika Kusini kuomba hifadhi wameitaka serikali ya nchi hiyo kufanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma za maofisa usalama wa Zimbabwe kuwatesa viongozi hao.

Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilifunguliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu cha Southern Africa Ligitation, ililenga kufunguliwa mashtaka kwa maofisa usalama wa Zimbabwe waliosafiri nchini humo kuchunguzwa kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Mnamo mwaka elfu 2007 kabla na baada ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe maofisa usalama nchini Zimbabwe wanadaiwa kuvamia ofisi za makao makuu ya chama cha MDC na kuwakamata baadhi ya wanachama na baadae kuwatesa ili watoe mipango ya chama.

Tayari serikali ya Zimbabwe imekanusha kuhusika na unyanysaji huo ikisema kuwa kesi hiyo inalenga kuichafua serikali inayoongozwa na rais Robert Mugabe.

Mawakili wa upande wa utetezi wamedai kuwa kwa vile nchi ya Afrika Kusini ni mwanachama wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC inawajibu wa kuchunguza tuhuma zozote ambazo zinaashiria kuwa kulikuwepo na ukiukwaji wa haki za binadamu na nyanyasaji wa kijinsia.

Wananchi waliofungua kesi hiyo wameorodhesha majina ya maofisa 17 wa usalama wa taifa nchini Zimbabwe ambao wanadaiwa kuwa walishiriki kwenye mpango wa kuwakamata na kuwatesa wananchi waliokuwa wakiunga mkono upinzani.

Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Hans Fabrcius amesema kuwa maofisa wa upelelezi wa Afrika Kusini walikiuka katiba na sheria za nchi ambazo ni wazi ziliwataka kuchunguza tuhuma hizo na kuwafikisha mahakamani watu waliotuhumiwa.