Mali

Raia wa Kaskazini mwa Mali waunda Umoja kupambana na Makundi ya Kiislam na Waasi wa Tuareg

Kiongozi wa Jeshi lililopindua Serikali ya Mali, Kapteni Amadou Sanogo.
Kiongozi wa Jeshi lililopindua Serikali ya Mali, Kapteni Amadou Sanogo. Reuters/Luc Gnago

Raia waishio Kaskazini mwa Nchi ya Mali wanajiandaa kupinga kundi la kiislam na waasi wa kundi la Tuareg ambao wamekuwa wakidhibiti miji ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Chama cha wakazi wa eneo hilo, COREN limetoa kauli kuwa, Raia wameamua kuungana wenyewe kwa kile walichodai kuwa ni baada ya kukosa utetezi kutoka mamlaka za kisiasa na kijeshi.

Umoja wa COREN, unaounganisha makundi na Vyama mbalimbali umewahakikishia wakazi wa eneo la kaskazini kuwa litawaunga mkono na kuwataka Raia kupambana kwa kila namna huku ukitoa wito kwa mamlaka kutekeleza majukumu yao.

Mji wa Gao hii leo ulirejea katika hali ya Utulivu asubuhi ya Leo baada ya mapigano wakati wa maandamano yaliyofanywa jana na Raia dhidi ya makundi ya waislamu wenye msimamo mkali na wenye silaha ambao waliudhibiti Mji huo kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu.

Takriban watu watano walijeruhiwa siku ya Jumatatu, mmoja akijeruhiwa kwa Risasi baada ya watu wenye silaha kufyatua risasi hewani na katika kundi la watu.

Mali moja ya nchi zilizoheshimika kwa mafanikio ya historia ya kuheshimu utawala wa Kidemokrasia, iliingia katika machafuko tarehe 22 mwezi March baada ya Jeshi la Nchi hiyo kuuangusha utawala wa Rais wa Nchi hiyo, Amadou Toumani Toure ambae alishutumiwa yeye na Serikali yake kuwa haikuwa ikifanya juhudi za kutosha kupambana na waasi wa Tuareg kaskazini mwa nchi hiyo.