Vikosi vya Congo vyashambulia Ngome ya Waasi Mashariki mwa Nchi hiyo
Imechapishwa: Imehaririwa:
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC limeshambulia ngome zinazoshikiliwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo na kuchangia kuzuka kwa mapigano makali baina yao hatua iliyowafanya wakazi kukimbia maeneo hayo.
Mashambulizi makali yameshuhudiwa katika eneo la safu za milima Mbuzi na Tchanzu zilizopo Kaskazini mwa Jimbo la Kivu ambapo wanajeshi wa serikali ya DRC waliamua kuwafungia kazi waasi.
Waasi hao ni askari ambao wameasi katika jeshi na kuendelea kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria ikiwemo ni pamoja na kuua wananchi sambamba na kuendesha ubakaji kwa wasichana na kinamama.
Waasi hao wanaelezwa wapo mamia na wamekuwa wakiweka kambi katika eneo la mpaka wa Rwanda na Uganda hasa huko Rutshuru pamoja na eneo la Mbuga za Taifa za Wanyama za Virunga.
Mashambulizi haya yanakuja wakati huu ambapo Jeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC likiendelea na msako wa mbabe wa kivita Jenerali bosco Ntaganda ambaye anasakwa kwa udi na uvumba na Mahakama ya ICC.