CONGO

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yatumia makomandoo kupambana na waasi

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetuma makomandoo wa kijeshi ili kuongeza nguvu katika majeshi yanayokabiliana na na majeshi ya waasi katika eneo la Kivu Kaskazini. 

Matangazo ya kibiashara

 Maafisa wa jeshi wamesema kuwa wameongeza kikosi hicho kipya katika jeshi la kawaida kwa ajili ya kuwasaka waasi ambao wanaonyesha kuleta upinzani dhidi ya majeshi yao karibu na mipaka ya Uganda na Rwanda.

Maafisa hao wamesema kuwa vikosi vipya viwili vimewasili huku vikiwa na makomandoo hao na ndani ya siku mbili watahakikishwa wanarejesha katika himaya yao maeneo yaliyo katika mikono ya waasi.

Mapigano mapya yalizuka baina ya majeshi ya serikali na waasi wa kundi la M23 huko Kivu Kaskazini katika mbuga moja ambayo ni makazi ya wanyama aina ya nyani ambao wanaonekana kuwa katika hatari.

Waasi hao ni sehemu ya waasi ambao mwaka 2009 waliingizwa katika majeshi ya serikali kutokana na makubaliano ya amani lakini wameamua kuasi tena kwa madai kuwa wamekuwa hawatendewi haki inavyopaswa.

Serikali hiyo Kongo imekuwa ikimshutumu kiongozi wa zamani wa waasi Bosco Ntaganda kwa kuongoza uasi na sasa anasakwa na mahakama ya uhalifu wa kivita, ICC kwa kuingiza watoto katika vita madai ambayo yeye amekuwa akiyakanusha.