Senegal

Senegal kuwania uandaaji wa fainali Kombe la Mataifa Afrika 2019

RFI/David Kalfa

Senegal imetangaza rasmi kuwa itawania uandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa la Afrika za mwaka 2019 na inaona huo utakuwa wakati muafaka wa kufanya hivyo na kujijengea heshima katika medani ya michezo hususan soka.

Matangazo ya kibiashara

Senegal kwa mara ya kwanza iliandaa mashindano hayo kunako mwaka wa 1992 na sasa inajipanga kufanya hivyo muda huo utakapofika.

Waziri wa michezo wa Senegal El Hadj Malick Gackou amesema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akifanya kazi na shirikisho la soka la nchi hiyo ili fainali hizo za mwaka 2019 zifanyike katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Waziri huyo amesema kuwa tayari ameshafanya mazungumzo kujadili suala hilo na rais wa CAF, Issa Hayatou na hiyo itakuwa sehemu ya mpango maalum wa Senegal wa kufikia mwaka 2020 nchi hiyo iwe imewekeza katika michezo kwa kuibua vipaji kuanzia ngazi ya chini.

Aidha mpango unalenga kuwekeza katika miundombinu ya michezo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Afrika Kusini itaandaa fainali za mwaka 2013 wakati Morroco itaandaa fainali za mwaka 2015 ambapo Afrika Kusini ilibadilishana na Libya ambayo sasa itaandaa fainali za mwaka 2017 kutokana na hali ya vita nchini humo.