Zoezi la kuhesabu kura linaendelea baada ya uchaguzi wa siku mbili nchini Misri
Imechapishwa: Imehaririwa:
zoezi la kuhesabu kura zilizopigwa nchini Misri linaendelea hii leo baada ya siku mbili za uchaguzi wa Urais wa kwanza kufanyika tangu kuanguka kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.
Raia wa Misri takriban milioni 50 walipewa nafasi ya kupiga kura kuchagua kati ya wagombea 12 uchaguzi ambao umefanyika katika hali ya utulivu, pasina kuripotiwa vitendo vya udanganyifu.
Tume ya uchaguzi imesema asilimia 50 imepiga kura katika siku mbili za uchaguzi.
Chama chenye nguvu nchini humo, Muslim Brotherhood kimetabiriwa kuwa mgombea wake Mohammed Mursi atakuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani ameipongeza Misri kwa kufanikisha uchaguzi wa kihistoria na kuahidi kufanya kazi na itakayokuwa Serikali ya Cairo wakati taifa hilo litakapokuwa likijenga demokrasia, desturi, tamaduni na kuheshimu haki za binaadam.
Majibu ya kura nchi nzima yanatarajiwa kutoka hii leo lakini matokeo Rasmi yatatolewa tarehe 27 mwezi huu.
Baraza la kijeshi nchini humo lililokuwa madarakani tangu kuondoka kwa Mubarak, limeahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa Kiraia mwishoni mwwa mwezi June baada ya kupatikana Rais.