KENYA

Mtu mmoja anahofiwa kupoteza maisha na wengine 20 wakijeruhiwa nchini Kenya kwenye mlipuko

Moto ambao unateketeza maduka Jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kutokea mlipuko mkubwa mchana huu
Moto ambao unateketeza maduka Jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kutokea mlipuko mkubwa mchana huu

Mtu mmoja anahofiwa kupoteza maisha na wengine sihirini kujeruhiwa nchini Kenya baada ya kutokea mlipuko mkubwa unaoelezwa kuwa ni wa bomu uliotokea katikati ya Jiji la Nairobi lililotekelezwa na watu ambao bado hawajabainika lakini Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab linahusishwa.

Matangazo ya kibiashara

Mlipuko huo mkubwa unaelezwa kutokea mchana majira ya saa saba na kuharibu miundombinu sambamba na maduka huku watu kadhaa ambao walikuwepo kwenye eneo hilo wakijeruhiwa wengine wao vibaya.

Majengo yaliyo karibu na eneo lililoshambuliwa yameshika moto na kuongeza hofu katika mtaa huo uliotawaliwa na shughuli za biashara kitu ambacho kimezidisha hofu ya usalama katika nchi hiyo iliyovitani kupambana na Wanamgambo wa Al Shabab.

Kundi la Al Shabab limeingia lawamani kwa mara nyingine kutokana na lenyewe kutajwa kutekeleza mashambulizi mara kwa mara dhidi ya Kenya kitendo ambacho serikali ya Nairobi kiliwasukuma na kuamua kulivanhia njuga Kundi hilo na kutaka kulisalimisha.

Jeshi la Polisi nchini Kenya tayari limesema ni Al Shabab ambao wametekeleza shambulizi hilo licha ya kwamba wanaendelea na uchunguzi ambapo watatoa taarifa kamili huku idadi ya watu sita wakitaja kujeruhiwa hadi sasa.

Shambulizi hili linakuja mwezi mmoja baada ya Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab kusema watafanya shambulizi la kulipiza kisasi kutokana na operesheni ya Jeshi la Kenya inayofanywa ikiwa na jina la Linda Nchi.

Kikosi cha Msalaba Mwekundu na Zimamoto wameendelea kutoa huduma kwa wananchi waliojeruhiwa pamoja na kuzima moto uliotokea kutokana na shambulizi hilo la bomu lililotokea Jijini Nairobi.

Waathirika wakubwa ni wafanyabiashara ambao wamepata uharibifu wa mali zao kutokana na moto uliozuka kuleta madhara makubwa na Polisi imeahidi kutoa taarifa kamili juu ya uhalifu ambao umetokea.

Jeshi la Kenya lililazimika kuingia nchini Somalia kukabiliana na Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab ambalo liliendesha utekaji wa watalii ambao walikuwa wanatembelea eneo la Pwani.