JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-DRC

Serikali ya DRC yakataa kufanya mazungumzo na Waasi huku Umoja wa Mataifa UN ukisema Rwanda inafadhili waasi hao

Mwanajeshi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC akiwa kwenye doria kwenye eneo la mpaka wa nchi hiyo na Rwanda
Mwanajeshi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC akiwa kwenye doria kwenye eneo la mpaka wa nchi hiyo na Rwanda

Umoja wa Mataifa UN umesema unaushahidi wa kutosha wa kudhihirisha namna ambavyo serikali ya Rwanda inavyowasaidia waasi wanaopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC wakati huu ambapo mapigano makali yakiendelea kushuhudiwa na serikali ya Kinshasa ikisema haiwezi kujadilia chochote na waasi.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Umoja wa Mataifa UN imeeleza wanajeshi ambao wanaasi kutoka Jeshi la DRC wamekuwa wakipatiwa mafunzo pamoja na silaha kutoka serikali ya Rwanda ambayo imekuwa wafadhili wakubwa wa mapigano na machafuko ambayo yanashuhudiwa mashariki mwa nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa UN imesema tangu kuzuka kwa mapigano mapya mwezi April katika eneo la Mashariki mwa DRC nchi jirani ya Rwanda imekuwa mstari wa mbele kufadhili waasi ambao wanapambana na serikali iliyopo madarakani.

Ripoti hii inakuja wakati serikali ikisema kamwe haiwezi kukaa meza moja na waasi nchini humo kwa ajili yakujadiliana na badala yake itatumia nguvu za kijeshi katika kuwasambaratisha na kukomesha mauaji ambayo yamekuwa yakishuhudiwa.

Kundi la Waasi la M23 limelalamika kuendelea kushambuliwa na majeshi ya serikali ya DRC wakati lenyewe limekuwa tayari kufanya mazungumzo na serikali ili kupata suluhu na hatimaye wapiganaji wao wajiunge na jeshi la serikali.

Serikali ya Kinshasa imesema waasi wa M23 hawana nidhamu kwani walipewa muda wa kujisalimisha lakini wakakaidi amari hiyo na kuendelea kufanya mashambulizi Mashariki mwa DRC kitu kilichowasukuma kutumiwa Makomandoo kuwasambaratisha.

Msemaji wa Kundi la M23 Vienney Kazarama amethibitisha kuendelea kushambuliwa na Jeshi la DRC lakini hata hivyo bado wao wanashikilia eneo la Mbuzi huku wakiendelea kusisitiza kuwa tayari kufanya mazunbumzo na serikali.

Waasi wa M23 ambao wengi wao ni wanajeshi waliojiondoa katika Jeshi la Taifa wamekuwa mstari wa mbele kupambana na serikali tangu mwezi uliopita na wakishutumiwa kumhifadhi Mbabe wa Kivita ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC Jenerali Bosco Ntaganda.

Serikali ya DRC imejiapiza kuyamaliza na Makundi yote ya waasi ambayo yameendelea kufanya uhalifu Mashariki mwa nchi hiyo sambamba na kumkatama Jenerali Ntaganda na kisha kumfikisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC.