SUDAN-SUDAN KUSINI

Sudan Kusini yaituhumu Sudan kuishambulia siku moja kabla ya kuanza upya kwa mazungumzo yao

Sudan Kusini imesema majirani zao wa Sudan wamefanya mashambulizi kwa kutumia ndege za kivita na kulenga maeneo yenye utajiri wa mafuta ambayo yamechangia kuzusha hali ya mtafaruku baina ya nchi hizo tangu Juba ijitangazie uhuru wake kutoka Khartoum.

Mpatanishi wa Sudan Kusini kwenye mgogoro baina yao na Sudan Pagan Amum akizungumza na wanahabari kueleza hatua zilizofikiwa
Mpatanishi wa Sudan Kusini kwenye mgogoro baina yao na Sudan Pagan Amum akizungumza na wanahabari kueleza hatua zilizofikiwa Reuters / Z. Bensemra
Matangazo ya kibiashara

Mpatanishi Mkuu kwenye mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini kutoka Juba Pagan Amum amesema kuwa jirani zao wa Sudan wamefanya mashambulizi kwenye eneo la mpaka wa nchi hizo mbili huku pia wakiendelea kupeleka vikosi vyao kufanya mashambulizi zaidi.

Kauli hii inakuja huku Dunia ikisubiri kwa hamu kuanza kwa mazungumzo baina ya nchi hizo mbili ambayo yamepangwa kufanyika kesho chini ya Mpatanishi wa Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki.

Mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuwaleta kwenye meza ya mazungumzo Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na mwenzake Rais Omar Hassan Al Bashir wa Sudan yamekuwa yakivurugika kila mara kutokana na kuzuka mapigano baina ya pande hizo.

Mapema serikali ya Sudan imewasilisha malalamiko mapya kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN wakiituhumu Sudan Kusini kwa kufadhili waasi ambao wamekuwa wakileta machafuko huko Khartoum.

Kuwasilishwa kwa malalamiko hayo mapya kwenye Baraza la Usalama kunaonekana kama moja ya kikwazo kingine kabla ya kuanza kwa mazungumzo baina ya nchi hizo mbili jirani yaani Sudan na Sudan Kusini.

Juma lililopita Mpatanishi wa mgogoro kati ya Sudan na Sudan Kusini ambaye ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mbeki alifanikiwa kuwashawishi viongozi wa nchi hizo mbili kurejea kwenye mazungumzo na kwa pamoja wakaridhia hilo.

Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini ulizidi kushika kasi baada ya kila upande kutangaza uhalali wa kumiliki eneo lenye utajiri wa mafuta la Heglig kitu ambacho Umoja wa Mataifa UN ulilazimika kutolea ufafanuzi na kusema Juba wanakalia kwa nguvu eneo hilo linastahili kumilikiwa na Khartoum.

Mazungumzo hayo yanayoanza upya siku ya jumanne yanatarajiwa kutoa mwanga halisi kuhusu hatima ya uhusiano wa nchi hizo mbili zenye mgonano mkubwa wa kimipaka sambamba na kuwania umiliki wa maeneo yenye utajiri mkubwa wa visima vya mafuta.