SUDAN-SUDAN KUSINI-ETHIOPIA

Mazungumzo baina ya Sudan na Sudan Kusini yanaanza huku Khartoum ikiondoa vikosi vyake Abyei

Mpatanishi wa Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini kutoka Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki ataongoza mazungumzo mapya huko Ethiopia
Mpatanishi wa Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini kutoka Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki ataongoza mazungumzo mapya huko Ethiopia Reuters/Phil Moore

Wajumbe kutoka Sudan na Sudan Kusini wanakutana kwa mara nyingine Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia chini ya Mpatanishi wa Umoja wa Afrika AU kwenye mgogoro wa mipaka unaogubika nchi hizo mbili Thabo Mbeki kuanza upya mazungumzo yao baada ya awli kuvunjika.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe hao kutoka kila upande wanakutana lengo likiwa ni kumaliza mgogoro wa mipaka pamoja na umiliki wa maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ambao umekuwa chanzo cha machafuko baina ya nchi hizo mbili tangu zimejitenga mwaka jana mwezi Julai.

Mazungumzo haya yanasimamia na Umoja wa Afrika AU chini ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mbeki yanaangaliwa kama fursa nyingine adhimu kwa majirani hao kuhakikisha wanafikia muafaka wa mfarakano wao ambao umedumu kwa miezi karibu tisa sasa bila ya kupatiwa suluhu.

Mbeki ndiye ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa katika kuhakikisha suluhu inafikiwa baina ya nchi hizo mbili baada ya kufanya ushawishi kwa Rais wa Sudan Omar Hassan Al Bashir na mwenzake wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Pande zote ambazo zinakinzana zimetuma wawakilishi wake nchini Ethiopia kwa lengo la kushirikia kwenye juhudi hizo za kupata suluhu ya kudumu na kumaliza mapigano ya kila mara kwenye eneo la mipaka.

Mazungumzo haya yanarejea tena huku Msemaji wa Jeshi la Sudan Sawarmi Khaled Saad akinukuliwa akithibitisha majeshi yao yataondoka kutoka Jimbo lenye machafuko la Abyei hii leo baada ya kuwepo kwa shinikizo la Umoja wa Mataifa UN.

Khaled amesema wamefikia uamuzi wa kuondoa majeshi yao Abyei ikiwa ni mwaka mmoja tangu waweke vikosi vyao katika eneo hilo ambalo limekuwa likishuhudia machafuko na vifo vya raia.

Msemaji huyo wa Majeshi ya Sudan amesema wanaondoa vikosi vyao baada ya Mpatanishi wa mgogoro Mbeki kuwataka wafanye hivyo ili mazungumzo hayo mapya yasikutane na vipangamizi na hatimaye yakavunjika tena.

Hali ya sintofahamu ilizuka baina ya nchi za Sudan na Sudan Kusini baada ya mgogoro wa kugombea maeneo yenye utajiri wa mafuta kuzuka hasa kule Heglig ambapo kila upande ulijinadi kuwa na mamlaka na eneo hilo.