SOMALIA

Rais wa Somalia Ahmed anusurika kifo baada ya Al Shabab kushambulia msafara wake akiwa ziarani Afgoye

Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed amenusurika kifo kwenye shambulizi lililolenga msafara wake wakati akizuru Afgoye
Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed amenusurika kifo kwenye shambulizi lililolenga msafara wake wakati akizuru Afgoye REUTERS/Murad Sezer

Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed amenusurika kifo baada ya Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab kutekeleza shambulizi lililolenga msafara wake lakini Maofisa wa serikali wamethibitisha amefanikiwa kutoka bila ya kuumia.

Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hili limewajeruhi wanajeshi wawili wa Somalia baada ya watu wenye silaha wanaotajwa kuwa wanachama wa Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab walipofyatua risasi kulenga msafara huo wa Rais Ahmed.

Msafara wa Rais Ahmed ulikuwa unaeleka katika eneo la Afgoye ambalo kwa sasa Jeshi la Umoja wa Afrika AMISOM pamoja na Jeshi la Serikali limetangaza kulishikilia baada ya kujigamba kuwatimua Wanamgambo wa Al Shabab.

Afisa wa Jeshi Mohamed Moalim amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo lililolenga msafara wa Rais Ahmed na limetokea wakati Kiongozi huyo akifanya ziara kwenye eneo la Afgoye kujionea operesheni inayofanywa na serikali.

Moalim ameendelea kusema kuwa Rais Ahmed anaendelea vyema kabisa licha ya kutokea kwa shambulizi hilo lililolenga msafara wake lakini mwenyewe hajajeruhiwa kwenye tukio hilo la kushtukiza.

Msafara huo ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa Majeshi ya AMISOM na yake ya Serikali ambayo yamefanikisha kuuchukua mji wa Afgoye kutoka kwenye makucha ya Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab waliokuwa wameweka kambi.

Mtandao ambao unaliunga mkono Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab umesema kuwa Kundi hilo limetekeleza shambulizi dhidi ya Mkuu wa Maadui ambaye ni Rais Ahmed ambaye alikuwa anazuru Afgoye.