LIBERIA-SIERRA LEONE-UHOLANZI

Hukumu ya Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor kutolewa hii leo kwa kufadhili vita nchini Sierra Leone

Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor anatarajiwa kusomewa hukumu yake leo mbele ya Mahakama Maalum inayosikiliza Makosa ya Uhalifu nchini Sierra Leone SCSL baada ya kukutwa na hatia ya makosa kumi na moja ya uhalifu ambayo aliyatenda nchini Sierra Leone kwa kuwafadhili waasi ambao walisababisha vifo vya wananchi wengi wasio na hatia.

Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor akiwa kwenye Mahakama Maalum inayosikiliza makosa ya Kivita ya Sierra Leone SCSL
Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor akiwa kwenye Mahakama Maalum inayosikiliza makosa ya Kivita ya Sierra Leone SCSL
Matangazo ya kibiashara

Mahakama Maalum inayosikiliza makosa ya uhalifu ya nchini Sierra Leone SCSL itatoa hukumu hiyo kwa Taylor ambaye amekutwa na hatia ya kufadhili waasi ambao walikuwa wanampatia madini ikiwemo almasi na dhabahu kisha yeye anawapatia silaha za kupambana na serikali.

Taylor anatarajiwa kukabiliwa na kifungo ambacho huenda kikamfanya amalize maisha yake yote akiwa jela kutokana na hukumu ambayo itakayotolewa kuwa si chini ya miaka ishirini na tano kwa makosa kumi na moja ambayo aliyatenda nchini Sierra Leone kwa kufadhili uhalifu mkubwa uliotendeka.

Hukumu hiyo itamfanya Taylor kuwa Kiongozi wa kwanza wa nchi kuhumukiwa chini ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC yenye makao yake huko The Hague nchini Uholanzi kwa makosa ya uhalifu aliyoyatenda akiwa madarakani.

Mwendesha Mashtaka Brenda Hollis alitoa pendekezo la kifungo cha miaka themanini kwa Taylor ambaye amekutwa na hatia ya makosa kumi na moja kwenye vita ya miaka kumi ya yenyewe kwa wenyewe iliyoshuhudiwa nchini Sierra Leone.

Taylor alikutwa na makosa kumi na moja tarehe ishirini na sita ya mwezi April baada ya ushahidi kudhihirisha alilifadhili Kundi la Waasi la RUF ambalo liliendesha vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha vifo vya watu laki moja na elfu ishirini.

Taylor alikuwa akitoa silaha kwa Kundi la Waasi la RUF ambalo lenyewe lilikuwa likimpatia almasi huku Kundi hilo likiendelea kutekeleza ubakaji na mauaji sambamba na kuajiri watoto wenye chini ya umri wa miaka kumi na tano kwenye jeshi lao.

Hukumu hiyo ikitolewa dhidi ya Taylor atatumikia kifungo chake nchini Uingereza huku majaji wakibanwa na kifungo cha kutomhukumu kifungo cha maisha na badala yake watalazimika kusema atafungwa kwa miaka mingapi.

Taylor kwenye ushahidi wake ambao aliotoa kwenye Mahakama ya SCSL alisema kuwa hongo ilitumika kwa mashahidi ili waweze kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake na ukweli ni kwamba yeye hajahusika na kufadhili vita hivyo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone vilizuka mwaka 1991 na kutamatika mwaka 2001 ambapo watu wengi wameathiriwa kwa kubakia na ulemavu wa maisha sambamba na wengine 120,000 kupoteza maisha.