SUDAN-SUDAN KUSINI-ETHIOPIA

Mazungumzo ya Sudan na Sudan Kusini yaingia siku ya pili huku UN ikithibitisha Khartoum kuondoa majeshi yake Darfur

Mpatanishi wa Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini kutoka Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki akiendelea kuongoza mazungumzo mapya huko Ethiopia
Mpatanishi wa Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini kutoka Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki akiendelea kuongoza mazungumzo mapya huko Ethiopia AFP/ Kambou Sia

Mazungumzo ya kusaka suluhu ya mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini yanaingia siku ya pili hii leo nchini Ethiopia chini ya Mpatanishi wa Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki huku Umoja wa Mataifa UN ukithibitisha serikali ya Khartoum kuondoa majeshi yake katika Jimbo lenye machafuko la Darfur.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo hayo yameshuhudia serikali ya Khartoum ikiendelea kujiapiza ipo tayari kupata suluhu ya mgogoro huo na kuondoa tofauti zilizopo baina yao na Sudan Kusini kitu ambacho kimechangia uwepo wa hali tete kiusalama.

Wajumbe kutoka pande zote wamekuwa na mazungumzo yenye kuonesha mwelekeo mwema katika siku ya kwanza chini ya Mbeki ambaye ameendelea kuhimiza wakati umefika wa kupatikana kwa suluhu ya mgogoro wa mipaka uliopo.

Sudan imesema kuwa inamatumaini makubwa mazungumzo haya ambayo yanafanyika nchini Ethiopia yatafungua ukurasa mpya wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili kutokana na uwepo wa mgogoro uliochangia hofu ya kiusalama.

Kwa upande wake Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amekiri haya ni majadiliano ya kipekee ambayo yanastahili kumaliza hali tete ambayo imekuwa ikishuhudiwa na kurejesha amani na urafiki mwema ambao umetoweka.

Mazungumzo haya ni matokeo ya ushawishi uliofanya na Mbeki kwa viongozi wa Sudan na Sudan Kusini lakini Umoja wa Mataifa UN nao ulitishia kuweka vikwazo kwa nchi hizo iwapo zisingemaliza tofauti zao na mapigano yaliyokuwa yanaeleka kubaya.

Wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo wanaongozwa na Idriss Mohammed Abdel Qadir kutoka Sudan na kwa upande wa Sudan Kusini wanaongozwa na Pagan Amum chini ya usamamizi wa Umoja wa Afrika AU kupitia mpatanishi wake Thabo Mbeki.

Mazungumzo haya yanaweza yakawa yamepata nguvu zaidi kwani Sudan imeondoa wanajeshi wake mia tatu ambao walikuwepo kwenye Jimbo lenye machafuko la Darfur kitu ambacho kilikuwa kinaonekana kama kikwazo cha kufikia makubaliano.