MISRI

Mubarak na wanawe kujua iwapo wanahatia ya mauaji na ulaji wa rushwa siku ya Jumamosi

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak akiwa chini ya ulinzi mkali wakati akiwasili Mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak akiwa chini ya ulinzi mkali wakati akiwasili Mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili REUTERS/Stringer

Rais aliyeangushwa nchini Misri Hosni Mubarak pamoja na watoto wake Alaa na Gamal pamoja na Wakuu wa Usalama nchini humo wanatarajiwa kujua hatima yake iwapo watakutwa na hatia ya kutenda makosa ya mauaji na ulaji wa rushwa ambayo aliyatenda wakati akiwa madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama Kuu nchini Misri inatarajiwa kutoa ushahidi wa mwisho na iwapo imemkuta na hatia Mubarak pamoja na watoto wake kwa makosa ya mauaji na ulaji wa rushwa ambayo yanatajwa yalichangia kwa kiasi kikubwa kuondolewa madarakani kwa utawala wake kwa nguvu ya umma.

Mashtaka dhidi ya Mubarak yalifunguliwa rasmi mwaka jana mwezi August ikiwa ni miezi sita baada ya kuangushwa kwa utawala wake kupitia maandamano yaliyoitishwa nchi nzima kushinikiza kuondoka madarakani kwa kiongozi huyo aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili.

Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya ulaji wa rushwa na uuaji wa waandamanaji wakati wa machafuko yaliyoanza mapema mwaka jana ambapo yeye na watoto zake Alaa na Gamal pamoja na Viongozi wajuu saba wa Usalama ambao nao wanahusishwa na kutekeleza mauaji hayo.

Maandamano hayo yalichangia vifo vya watu mia nane na hamsini baada ya siku kumi na nane za maandamano yakushinikiza kujiuzulu kwa Rais Mubarak kwa kile ambacho wananchi walikuwa hawaridhishwi na utendaji wa serikali sambamba na kuendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Uamuzi wa Mahakama unasubiriwa wakati watoto wa Mubarak ambao ni Alaa na Gamal wakifunguliwa kesi nyingine inayowatuhumu wao kuhusika kwenye kashfa ya ufisadi ambayo wameitenda kwenye soko la hisa nchini humo.

Alaa na Gamal wanahukumiwa kwa kosa la ufisadi kwenye soko la hisa pamoja na watu wengine saba ambao wanatajwa kushirikiana nao kwenye tuhuma hizo ambazo ziliwanufaisha wao.

Kesi hiyo ya ufisadi ambao inawakabili Alaa na Gamal pamoja na watu wengine saba inatarajiwa kuanza kusikilizwa katika Mahakama nchini misri siku ya Jumamosi ambayo itakuwa ni tarehe mbili ya mwezi Juni.