SOMALIA-UTURUKI

Uturuki yaandaa Mkutano wa kujadili namna ya kuisaidia Somalia

Uturuki imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Somalia na imeshatoa $365m kwa misaada pamoja na vifaa
Uturuki imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Somalia na imeshatoa $365m kwa misaada pamoja na vifaa

Wawakilishi kutoka nchi wanachama hamsini na nne wamekutana katika Jiji la Istanbul nchini Uturuki kuangalia namna ya kulisaidia Taifa la Somalia kujijenga upya na kujiimalisha baada ya kushuhudia vita vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili sasa katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Wawakilishi hayo kwa pamoja wanaangalia ni kwa namna gani wanaweza kubadili nadharia ya kuiona Somalia kama nchi ambayo imeshindwa baada ya kuwepo kwenye vita ya zaidi ya miaka ishirini na kujadili ni kwa vipi usalama wake utatengamaa na hatimaye kuanza kujipatia maendeleo.

Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki Bekir Bozdag kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa pili unaofanyika Jijini Istanbul kwa ajili ya kusaidia Somalia amesema baada ya mgogoro wa muda mrefu umefika wakati wa kutumia fursa hii kwa ajili ya kuimarisha usalama na amani katika taifa hilo.

Bozdag ameendelea kusema hali ilivyo kwa sasa katika Jiji la Mogadishu ambalo ni ngome ya serikali imekuwa ni ya usalama na hivyo inafaa kwa jumuiya ya kimataifa kufungua biashara sambamba na kuongeza juhudi za kuijenga zaidi nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita hivyo kwa miongo miwili.

Mkutano huu wa siku mbili unaokuja baada ya ule ambao ulifanyika Jiji London nchini Uingereza umeanza kwa mazungumzo baina ya maofisa waandamizi juu ya masuala ya biashara na utaalam ambapo mada kuu nne zilikuwa ni maji, nishati, barabara na uendelevu wa nchi hiyo.

Siku ya Ijumaa Mkutano huo utajiegemeza kwenye mkwamo wa kisiasa mbao unaendelea kushuhudiwa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ni miongoni mwa watakaohudhuria pamoja na Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed.

Viongozi wengine ambao watahudhuria mkutano huo siku ya Ijumaa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambao ni wenyeji pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague.

Waziri Mkuu wa Somalia Abdiweli Mohamed Ali amewaambia wawakilishi wanaohudhuria mkutano huo ya kwamba hatima ya nchi yao ipo kwenye mikono ya wale wote ambao wanahudhuria mkutano humo muhimu.

Serikali ya Rais Ahmed imekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kuendelea kukabiliwa na upinzani kutoka Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi kwenye maeneo mbalimbali nchini humo.