JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-DRC-RWANDA

Serikali ya Rwanda yakanusha kuwafadhili waasi wanaopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Mapigano yanaendelea kushuhudiwa Mashariki mwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
Mapigano yanaendelea kushuhudiwa Mashariki mwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Serikali ya Rwanda imekanusha kutoa mafunzo na kufadhili silaha waasi wanaopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC Mashariki mwa nchi hiyo na kusemwa wamesikitishwa na ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa UN kuthibitisha ufadhili unaofanywa na Kigali.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikwabo amekanusha vikali nchi yake kufadhili waasi ambao wanapambana na serikali ya DRC na kusema ripoti ya Umoja wa Mataifa UN ni ya uongo na ina nia ya kuleta machafuko kwenye eneo lote la Maziwa Makuu kwa kuleta suala hilo.

Waziri Mushikwabo amesema nchi yake haiwezi kujiingiza kwenye harakati za kuleta machafuko kwenye eneo la Maziwa Makuu hivyo haiwezi kabisa kuthubutu kutoa mafunzo au kuwafadhili waasi kwenye nchi yoyote jirani ili wapambane na serikali iliyopo madarakani.

Serikali ya Rwanda inakanusha uhusika wake kuwafadhili Waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC wakati wapiganaji wa waasi wa Kundi la M23 wakithibitisha kupata mafunzo nchini Rwanda sambamba na kufadhiliwa kwa silaha.

Taarifa hiyo imekuja baada ya waasi kumi na moja kuthibitisha kufunzwa kijeshi nchini Rwanda na sasa wamekuwa mstari wa mbele kupambana na Jeshi la DRC katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Wapiganaji hao kumi na moja kutoka Kundi la Waasi la M23 ambao wamejiunga serikali wamesema walipatiwa mafunzo nchini Rwanda kabla ya kukabidhiwa kwa waasi ambao wakawa wanaendesha mapambano dhidi ya serikali.

Uwepo wa taarifa hii kumezidisha hofu juu ya hatima ya baadaye ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili kutokana na madai ya upande mmoja kusaidia waasi ambao wanapambana na serikali halali.

Mapema juma hili Umoja wa Mataifa UN ulitoa taarifa ikiituhumu serikali ya Rwanda kwa kutoa mafunzo pamoja na kufadhili waasi wanaopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwenye eneo la Mashariki.