Sudan

Maelfu ya raia wa Sudan Kusini kurejea nyumbani kufikia mwisho wa juma hili kutoka Sudan

Raia elfu 12 wa Sudan Kusini wanatarajiwa kurejea nyumbani kutoka Sudan kufikia mwisho wa wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la kimataifa linaloshughulika na maswala ya uhamiaji la  IOM limethibitisha kurudi nyumbani kwa raia hao wa Sudan Kusini ambao wamekuwa wakiishi katika mji wa Kosti, Kilomita 300 kutoka mji mkuu Khartoum kwa muda mrefu.

Serikali ya Khartoum inasema kuwepo kwa raia hao nchini humo kunahatarisha usalama wa taifa lao na ni sharti warudi kwao.

Muda wa mwisho wa raia hao wa Sudan Kusini wa kuondoka kabisa nchini Sudan wa tarehe 5 mwezi uliopita uliahirishwa baada ya umoja wa mataifa kuingilia kati.

Siku ya Jumatatu watu 11,020 wakitumia ndege 73 wamerudishwa nyumbani huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kufikia mwisho wa wiki hii.

Zaidi ya raia wa Sudan Kusini 350,000 wamekuwa wakiishi nchini Sudan kabla ya Sudan Kusini kujitangazia uhuru wake mwaka uliopita.

Wakati hayo yakijiri,mkutano wa kutafuta suluhu la kudumu kati ya mataifa hayo mawili unaendelea mjini Addis Ababa nchini Ethiopia,chini ya msuluhishi mkuu wa Umoja wa Afrika Thambo Mbeki rais wa zamani wa Afrika Kusini.

Baadhi ya maswala nyeti yanayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na usalama wa mipaka baina ya mataifa hayo mawili,ugawanaji wa mapato ya mafuta na swala la uraia hasa kwa wananchi wa Sudan Kusini wanaoishi Sudan.