Libya

Waliokuwa waasi nchini Libya wavamia uwanja wa ndege jijini Tripoli

Kundi la waliokuwa waasi nchini Libya limevamia uwanja wa kimataifa wa ndege jijini Tripoli wakiwa wamejitahami kwa silaha na kutatiza shuighuli za kutua na kupaa kwa ndege katika uwanja huo.

Matangazo ya kibiashara

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kundi hilo la waasi wa zamani wamesababisha wafanyikazi na abiria waliokuwa katika uwanja huo wa ndege kuchanganyikiwa na kuingiwa na wasiwasi  bila kufahamu lengo la uvamizi huo.

Hata hivyo,waasi hao wanasema wamevamia uwanja huo wa ndege kwa sababu wanataka kuachiliwa huru kwa kiongozi wao Abu Ajila al-Habshi aliyekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa usalama wa serikali ya mpito.

Uongozi wa serikali ya mpito unaendelea kukabiliwa na changamoto za kuwaunganisha tena wananchi wa Libya baada ya kuangusha utawala wa kiongozi wa zamani wa taifa hilo Muamar Kadhafi aliyeuawa mwaka uliopita.

Wito umekuwa ukitolewa kwa viongozi wa serikali ya mpito kuweka chini silaha  na kudumisha amani baada ya mapinduzi dhidi ya uongozi uliopita.

Baadhi ya waliokuwa wapiganaji  waliofanikisha kuangusha utawala wa Kadhafi wanahisi wametengwa baada ya uongozi mpya kuchua uongozi wa taifa hilo.

Uvamizi huu umetokea wakati Libya ikijiandaa  kuandaa uchaguzi wa wabunge 200 tarehe 19 mwezi huu.