NAIROBI

Uwanja wa ndege wa Jomokenyatta jijini Nairobi nchini Kenya wafunguliwa tena

Safari za ndege katika uwanja mkubwa wa ndege Afrika Mashariki na Kati wa Jomo Kenyatta jiji Nairobi nchini Kenya,zimerejelewa tena baada ya ndege ya abiria kutoka Misri iliyokuwa inatua kukosa mwelekeo, Jumatano asubuhi katika uwanja huo.

Matangazo ya kibiashara

Ndege hiyo namba 849 ilikuwa na abiria 123 ilikuwa inatua baada ya kuwasili Nairobi kutoka jijini Cairo,baada ya kushindwa kufuata  barabara ya ndege na kukwama lakini hakuna abiria yeyote aliyejeruhiwa katika mkasa huo.

Afisa wa Mawasiliano katika uwanja huo Dominic Ngigi amethibitisha kutokea kwa mkasa huo na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha ndege hiyo kushindwa kutua.

Ngingi ameongeza kuwa tayari juhudi zimeshafanywa na shughuli katika uwanja huo zimerejea kama kawaida na kuwapa afueni mamia ya wasafiri waliokuwa wamekwama jijini Nairobi.

Hapo awali,ndege zote zilizostahili kutua jijini Nairobi zilikuwa zimeelekezwa mjini Mombasa ,Entebbe nchini  Uganda na Dar es salaam Tanzania.