Sudan-Marekani

Marekani yataka wakimbizi wa Sudan Kusini kusaidiwa kurudi nyumbani

Marekani inatoa wito kwa mataifa mengine na mashirika ya Kimataifa kutoa misaada ili kusaidia kuwarudisha  maelfu ya raia wa Sudan Kusini nyumbani kutoka Sudan.

Matangazo ya kibiashara

Marekani inasema imetoa Dola Milioni 34 kusaidia kuwasafairisha wakimbizi hao kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa baada ya muda wao wa kuishi Sudan kukamilika.

Raia wa Sudan Kusini zaidi ya Laki Moja wanaishi katika jimbo la Blue Nile na Kordofan Kusini na wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kwa ukosefu wa maji safi ya kunywa, na chakula.

Tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na wakimbizi inatoa wito wa kupatikana na Dola Milioni 145 kuwasaidia wakimbizi hao kurejela makwao kwa kuwasafirisha na kuwapa mahitaji ya msingi kama matibabu.

Wakati hayo yakijiri,mazungumzo ya amani chini ya Umoja wa Afrika kati ya Sudan na Sudan Kusini yanaendelea mjini Addis Ababa Ethiopia, kuzungumzia tofauti kati ya matifa hayo mawili.

Miongoni mwa maswala nyeti yanayotafutiwa ufumbuzi katika mkutano huo ni pamoja na namna ya mataifa hayo yanavyoweza kugawana mapato ya mafuta, ikiwa ni pamoja na umiliki wa visima hivyo na halikadhalika umiliki wa mipaka kati ya mataifa hayo mawili.