MISRI

Wanasiasa nchini Misri waafikiana kuhusu uchaguzi wa wajumbe wa Kamati ya kuadika katiba mpya

Vyama vya kisiasa nchini Misri hatimaye vimekubaliana namna vitakavyochagua wajumbe 100 watakaokuwa na jukumu la kuandika katiba mpya.

Matangazo ya kibiashara

Maafikiano hayo yalifikiwa kati ya wawakilishi wa vyama 22 vya kisiasa na viongozi wa serikali ya kijeshi na kumaliza mjadala wa majuma kadhaa ni lini kamati hiyo ingebuniwa ili kuanza kwa mchakato huo.

Uchaguzi wa wajumbe hao unatarajiwa kufanyika siku ya Jumanne wiki ijayo kabla ya zoezi la kuanza kuandika katiba hiyo kuanza.

Mbali na wanasiasa,maafisa wa kijeshi, polisi, wawakilishi kutoka idara ya Mahakama, mashirika ya wafanyikazi na viongozi wa Kiislamu na Wakristo wa dhehebu la Coptic watajumuishwa katika kamati hiyo.

Kabla ya maafikiano hayo, uongozi wa kijeshi ulikuwa umetoa saa 48 kwa wanasiasa kuafikana la sivyo wangeteua wenyewe wajumbe wa kamati hiyo.

Wanasiasa wa Muslim Brortherhood wamekuwa wakishtumiwa na wanasiasa wengine kutaka kuthibiti kamati hiyo ya katiba suala ambalo lilizua mgawanyiko wa kisiasa nchini humo.

Misri inajiandaa katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais tarehe 16 na 17 mwezi huu kati ya mgombea wa Muslim Brotherhood Mohammed Mursi na aliyekuwa Waziri Mkuu katika uongozi uliopita,Ahmad Shafiq.