Kenya-Ajali

Kenya yaomboleza kifo cha waziri wa usalama George Saitoti

Waziri wa Usalama wa raia Georges Saitoti afriki katika ajali ya helicopta
Waziri wa Usalama wa raia Georges Saitoti afriki katika ajali ya helicopta Reuters/Thomas Mukoya

Rais wa Kenya Mwai Kibaki ametangaza siku tatu za kitaifa kuomboleza vifo vya Waziri wa Usalama wa ndani Profesa George Saitoto na Naibu wake Joshua Orwa Ojode pamoja na walinzi wao 2 na marubani 2, walioangamia jana Jumapili katika ajali ya ndege katika eneo la Ngong nje kidogo na jiji kuu Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Asubuhi hii rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wanatarajiwa kuongoza mkutano wa dharura wa baraza la Mawaziri kuzungumzia vifo vya maafisa hao wa serikali. Shughuli za mazishi ya viongozi hao huenda zikatangazwa baada ya kikao hicho

Profesa Saitoti na Jushua Orwa alifariki dunia jana siku ya Jumapili katika ajali ya ndege aina ya Helicopta katika msitu wa Ngong wakati walipokuwa katika safari yao ya kuelekea katika kanisa moja magharibi mwa Kenya kufanya harambee ya ujenzi wa kanisa katika eneo hilo.

Idara ya polisi nchini Kenya imesema uchunguzi utafanyika kujua sababu ya ajali hiyo, na balozi wa Marekani mjini Nairobi, amesema Marekani iko tayari kusaidia kwenye uchunguzi huo, ikiwa itahitajika.

Msemaji wa polisi alieleza kwamba inavoelekea kuanguka kwa helikopta hiyo lilikuwa tukio la ajali.

Saitoti alikuwa miongoni mwa wagombea wa urais nchini Kenya katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika mwakani, na aliwahi kuhudumu kama makamu wa rais na waziri wa fedha katika serikali ya rais wa zamani Daniel Arap Moi iliokamilika mwaka 2002. Alikuwa na umri wa miaka 67

Saitoti na Ojode watakumbukwa sana katika juhudi zao za kupambana na kundi la kigaidi la Al-shabab nchini Kenya ambalo linaendelea kutishia usalama wa nchi hiyo. Inaaminiwa kuwa waziri Saitoti alihusika na uamuzi wa jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka jana.

Kundi la Al-Shabab limenukunuliwa kupitia mtandao wa Twitter likisema kuwa limefurahia vifo hivyo.