KHARTOUM-SUDAN

Polisi nchini Sudan wamekabiliana na waandamanaji wanaopinga hatua za ubanaji matumizi

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir
Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir REUTERS/Stringer

Polisi mjini Khartoum nchini Sudan wamekabiliana na maelfu ya waandamanji waliokuwa wamekusanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo wakipinga mpango wa Serikali wa kubana matumizi.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo ambayo leo yameingia siku yake ya tatu yameshuhudiwa yakigeuka vurugu baada ya polisi wa kutuliza ghasia kuamua kuingilia kati kuwatawanya waandamanaji hao.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo huku wengine pamoja na polisi wakiripotiwa kujeruhiwa wakati wa makabiliano hayo.

Msemaji wa polisi kwenye wa Khartoum amethibitisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji hao na kuongeza kuwa serikali ilishapiga marufuku maandamano yoyote kufanyika mjini Khartoum.

Siku ya Jumatatu rais wa nchi hiyo Omar Hassa al-Bashir alitangaza nchi yake kutumia njia za ubanaji matumizi kwenye bajeti yake kwa lengo la kufufua uchumi wa taifa hilo ambao umeoneka kudorora.

Kauli ya rais Bashir imekuja kufuatia waziri wa fedha wa nchi hiyo kutangaza bajeti ya dola za marekani bilioni 2.4 ambayo itatumika kwa mwaka wa fedha 2012/2013 huku ikitarajiwa maelfu ya wananchi kupoteza ajira zao.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kuwa uchumi wa Sudan umeendelea kudorora toka nchi hiyo kujitenga na majirani zao wa Sudan Kusini huku sekta yake kuu ya uchumi ambayo ni mafuta ikiathirika kwa kiasi kikubwa.