Mamlaka nchini Libya yakanusha kumnyanyasa Waziri Mkuu wa zamani

RFI

Mamlaka nchini Libya zimekanusha vikali taarifa kuwa polisi wake wanamfanyia vitendo vya unyanyasaji aliyekuwa waziri mkuu kwenye serikali ya marehemu Kanali Muammar Gaddafi, Baghdad al-Mahamud.

Matangazo ya kibiashara

Wakili anayemtetea Al-Mahmud amewaambia waandishi wa habari kuwa mteja wake amekuwa akipigwa na polisi kwenye gereza ambako anashikiliwa na kwamba anahofia usalama na afya ya kiongozi huyo kutokana na vipigo vya mara kwa mara.

Moja wa madaktari ambao wanatembelea jela ambayo Al-Mahmud anashikiliwa amesema kuwa hakuna ishara wala dalili kuwa kiongozi huyo anapigwa ingawa amekiri kuwa kiongozi huyo anaugua ugonjwa wa kisukari.

Katika hatua nyingine mwanasheria wa Australia anyeshikiliwa na mamlaka nchini humo Melinda Taylor kwa mara ya kwanza amewasiliana na familia yake na kudai kuwa yuko salama.

Taylor alikamatwa na wenzake wawili Juni 6, mwaka huu wakati wakimtembelea mtoto wa marehemu Gadafi, Seif al-Islam kwa lengo la kumsadia ambapo polisi wanadai kuwa walikuwa wamebeba ujumbe maalumu toka kwa viongozi wa karibu wa utawala ulioangushwa.