TANZANIA

Wahamiaji 42 wa Ethiopia na Somalia wafariki ndani ya Kontena nchini Tanzania

RFI

Zaidi ya wahamiaji haramu 42 wanaodaiwa kuwa ni raia wa Ethiopia na Somalia wamekufa na wengine zaidi ya 50 wako kwenye hali mbaya kufuatia kukosa hewa kutoka kwenye kasha la kontena ambalo walikuwa wanasafirishwa nalo wakielekea Malawi.

Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo ambalo limetokea kwenye kijiji kimoja ndani ya mji mkuu wa Tanzania Dodoma, walitelekezwa na dereva ambaye baada ya kuona kuwa baadhi yao wamekufa aliacha gari na kukimbia kusikojulikana.

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Pereira Silima amethibitisha kushuhudia miili ya wahamiaji hao ambao amesema walifariki kutokana na kukosa hewa, maji na chakula kwa muda mrefu ndani ya kasha la kontena ambalo walikuwa wakisafirishwa.

Polisi kwenye mji huo wamesema wanaendelea na msako wa dereva aliyekuwa akiendesha lori hilo pamoja na mmiliki wake huku wakiendelea kuwashikilia na kuwahudumia wahamiaji wengine ambao wamesalimika.

Hii ni mara ya pili kutokea kwa tukio kama hili kwenye mkoa wa Dododma baada ya mwaka jana mwezi december wakimizi wakisomali zaidi ya 20 kupoteza maisha kutokana na kukosa hewa.