Misri

Rais wa Misri, Mohamed Morsi asema ataheshimu uamuzi wa Mahakama

Rais wa Misri, Mohamed Morsi
Rais wa Misri, Mohamed Morsi © REUTERS

Rais wa Misri Mohamed Morsi amesema ataheshimu uamuzi wa Mahakama dhidi ya uamuzi wake wa kuwataka wabunge kurudi kazini. 

Matangazo ya kibiashara

Jumapili iliyopita rais Morsi alitoa Agizo la wabunge kurudi kazini ili kuanza mchakato wa kuandika katiba mpya,Mwezi mmoja baada ya Mahakama ya kikatiba nchini humo kulivunja Bunge baada ya kubaini kuwa uchaguzi wa wabunge haukufuata sheria ya uchaguzi.

Siku Moja baada ya Mahakama kupinga Amri ya Morsi, Morsi amesema kuwa ikiwa Mahakama ya kikatiba inazuia Bunge kutimiza Wajibu wao, wataheshimu hilo kwa kuwa nchi hiyo inaongozwa na Sheria.

Juma lililopita Rais Morsi alitoa Amri kwa Bunge kuanza kazi yake akibatilisha Uamuzi wa Jeshi kulivunja Bunge hilo kwa kile kilichoamriwa na Mahakama kuwa Wabunge walikuwepo Madarakani kinyume na Taratibu na Sheria.

Uamuzi wa Morsi kulirejesha Bunge ulipongezwa na Wafuasi wake wanaoamini kuwa uamuzi wa Mahakama wa kulivunja Bunge ulikuwa wa Kisiasa, huku Wapinzani nao waking'aka kuwa Morsi amepitiliza Madaraka yake.

Kwa mujibu wa Katiba ya Mpito nchini Misri, iliyoundwa na Majenerali wa Kijeshi, waliochukua Madaraka baada ya kuanguka kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Hosni Mubarak, Jeshi lina Mamlaka ya Kuvunja Bunge.