ZANZIBAR

Meli yazama Zanzibar ikiwa na zaidi ya abiria 200

Meli moja inayomilikiwa na kampuni ya SEAGAL iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar Tanzania imezama katika bahari ya hindi baada ya kukumbwa na dhoruba kali na hatimaye kupinduka.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa jeshi la polisi visiwani Zanzibar meli hiyo iliondoka Dar es Salaam mchana na imepatwa na ajali hiyo huku ndani yake kukiwa na abiria zaidi ya 200.

Mpaka sasa bado kuna utata wa madhara yaliyotokana na ajali hiyo na waokoaji kutoka vikosi vya bandari, polisi na jeshi la majini wanafanya jitihada mbalimbali za uokoji ili kusaidia manusura wa ajali.

Polisi wanasaidiana na maafisa wengine wa uokozi kutafuta watu hao ambao hawajapatikana tangu kuzama kwa meli hiyo.

Mwezi Septemba mwaka uliopita,meli nyingine ya abiria  ilizama katika bahari Hindi ikitokea Dar es salaam na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Tanzania imekuwa ikikumbwa na visa vya ajali za meli jambo ambalo linazua maswali mengi kuhusu usalama wa safari za majini katika taifa hilo.

Mwandishi wa RFI Kiswahili amezungumza na msemaji wa jeshi la polisi visiwani Zanzibar Inspekta Mohamed Muhina.