LIBYA

Muungano wa vyama vya kisiasa nchini Libya washinda uchaguzi wa wabunge

Upigaji kura nchini Libya
Upigaji kura nchini Libya

Muungano wa vyama vya kisiasa nchini Libya umeshinda uchaguzi wa kwanza wa wabunge nchini humo tangu kuangushwa kwa utawala wa kiongozi wa zamani nchini humo, Kanali Muamar Kadhafi aliyeuliwa mwaka uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Muungano huo unaongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Mahmoud Jibril kimeshinda viti 39 huku kile chenye mrengo wa kiislamu kikipata viti 17 kati ya viti vyote 80 vilivyotengewa vyama vya kisiasa nchini humo.

Bunge la Libya litakuwa na wabunge 200, huku 120 wakiwa wamechaguliwa nje ya vyama vya kisiasa.

Waziri Mkuu Abdurrahim al-Keib amesema matokeo hayo yanaleta matumaini ya kuimarika kwa demokrasia nchini humo,huku akidokeza kuwa huu ni wakati wa raia wa Libya kusherehekea.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, kutakuwa na wiki mbili za kukata rufaa kabla ya wabunge hao kuanza kazi ya kuandika katiba nchini humo.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa amani licha ya visa vichache vya ghasia kushuhudiwa katika maeneo kadhaa nchini humo.