NIGERIA

Watu 40 wafariki kutokana na mafuriko nchini Nigeria

REUTERS/Afolabi Sotunde

Watu wanaokadiriwa kufikia arobaini wamepoteza maisha nchini Nigeria katika Jiji la Jos baada ya kunyesha mvua kubwa iliyosababisha uharibifu wa makazi zaidi ya mia mbili Shirika la Msalaba Mwekundu limethibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika Jimbo la Plateau Manasie Phampe amethibitisha kutokea kwa maafa hayo na kusema inawezekana madhara yakawa makubwa zaidi kutokana na mvua kuendelea kunyesha.

Mvua hiyo imesababisha madhara makubwa kwa sababu bwawa la Lamingo lilizidiwa na wingi wa maji kitu ambacho kilichangia kuvunjika kwa kingo zake na hivyo maji kuanza kusambaa katika maeneo jirani.

Mratibu wa Wakala wa Taifa wa Masuala ya Dharura NEMA Alhassan Danjuma Aliyu amesema wanaendelea kukabiliana na madhara ambayo yameendelea kujitokeza wakishirikiana na vikosi vya usalama vilivyopo kwenye uokozi.

NEMA imeshaanza kutoa misaada ya haraka kutoka kwa waathiriwa wa mafuriko hayo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahema kwa ajili ya malazi sambamba na chakula kikijumuisha na maji safi.