MAPUTO

Zimbabwe na Madagascar zajadiliwa mjini Maputo

Mkutano wa siku mbili wa marais wa mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC)  umeanza mjini Maputo nchini Msumbiji ajenda kubwa ikiwa ni kuijadili hali ya kisiasa nchini Madagascar na Zimbabwe.
 

Matangazo ya kibiashara

Mataifa hayo mawili yanajadiliwa wakati huu yakiwa katika harakati za kuandaa Uchaguzi Mkuu mwaka ujao, uchaguzi ambao unatarajiwa kuwa kipimo cha kukomaa kwa demokrasia katika mataifa hayo.

Mapema wiki hii, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alikuwa mjini Harare nchini Zimbabwe kukutana na viongozi wa kisiasa nchini humo kushinikiza uharakishwaji wa mabadiliko ya kisiasia nchini humo, ikiwemo upatikanaji wa katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani.

Tofauti za kisiasa kati ya rais wa Madagascar Andry Rajoelina na rais wa zamani Marc Ravalomanana pia zinazungumziwa katika mkutano huo baada ya wanasiaisa hao kushindwa kuafikiana mara mbili nchini Ushelisheli chini ya msuluhishi wao Jacob Zuma ambaye pia ni rais wa Afrika Kusini.

Madagascar inatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wake mkuu mwaka ujao na rais Rajoelina ambaye alimpindua Ravalomanana mwaka 2009 ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Afrika Kusini akipinga kusimama kwa rais huyo wa zamani kwa kile anachiokisema ni kutokana na makosa ya kisiasa.

Mbali na mzozo huo wa kisiasa, Muungano huo unajadili pia namna ya kuimarisha miundombinu kati ya mataifa hao 15  kurahihisha biashara kati yao.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na mwenzake wa Malawi Joyce Banda pia wanakutana kuzungumzia mzozo kati ya mataifa yao kuhusu mmiliki wa Ziwa Nyasa.