DR CONGO

Waasi wa M 23 watishia kuchukua mji wa Goma

Kundi la waasi la M 23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linaonya kuwa litachukua uthibiti wa mji wa Goma ikiwa serikali jijini Kinshasa haitawapa usalama wakaazi wa mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa kundi hilo Vianney Kazarama amesema kuwa ikiwa rais Joseph Kabila hatatuma wanajeshi kulinda usalama katika mji huo, basi wao watalazimika kuchukua hatua hiyo ili kuzuia mauaji yanayoripotiwa kutokea mjini humo.

Zaidi ya watu 20 wamekamatwa katika mjini Goma katika siku za hivi karibuni wakiwa na silaha kama bunduki na vilipuzi, silaha ambazo zinaelezwa kutumiwa na makundi ya watu wasiojulikana ma  kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa.

Mashirika ya kutetea haki za bindamu nchini humo yanakashifu kundi hilo la M 23 kwa kile wanachokisema kuwa madai yao hayana msingi wowote na badala yake wanazungumza siasa .

Omar Kavota naibu Mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika jimbo la Kivu Kaskazini anasema kuwa Jumuiya ya Kimatifa inastahili kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wake kuzuia makundi ya waasi kama M23 kuendelea kutishia maisha ya raia Mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi hilo la M 23 ambalo kwa sasa makaazi yake ni Rutshuru kilomita 30 kutoka mjini Goma linafadhiliwa na serikali ya Rwanda kwa mujibu wa tuhma za Umoja wa Mataifa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tuhma ambazo Rwanda imeendelea kupinga.