UGANDA-ZAMBIA

Golikipa wa The Cranes ataka ushindi dhidi ya Chipolopolo uwe zawadi ya miaka 50 ya uhuru

RFI

Golikipa namba moja wa timu ya taifa ya soka ya Uganda Dennis Onyango amesema kitendo cha kufungwa kwa bao moja kwa bila na timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo katika mchezo wa awali kinaiweka katika hali ngumu The Cranes.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo golikipa huyo amesema hakuna haja ya kukata tamaa bali the Cranes inatakiwa kucheza mchezo wa kushambulia ili waweze kupata ushindi katika mchezo wa marudiano utakaofanyika mwishoni mwa juma.

Mchezo huo utapigwa jumamosi na endapo The Cranes itafungwa ama kutoka sare ya aina yoyote itakuwa imezamisha matumaini ya kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2013 nchini Afrika Kusini.

Golikipa Dennis Onyango amesema timu yake ya The Cranes inaweza kushinda mchezo huo kwa anasikia kuwa Chipolopolo inautilia wasiwasi mchezo huo utakaopigwa nchini Uganda.

Amesema kuwa Zambia itashuka dimbani ikiwa imeweka mkakati wa kulinda goli lake hivyo Cranes wakishambulia zaidi wanaweza kupata ushindi katika mchezo huo muhimu kwa timu zote mbili.

Hata hivyo amesema pamoja na kushambulia The Cranes pia lazima ijilinde ili kuzuia washambuliaji wa Chipolopolo kupenya katika ngome yao kiurahisi na kupata mabao.

Mchezaji huyo ambaye pia ni mlinda mlango wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini amesema ushindi na hatimaye kufuzu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978 kwa The Cranes vinaweza kuwa zawadi ya miaka 50 ya uhuru wa Uganda na wananchi wake.