ALGERIA-MALI-MAREKANI

Marekani yaiangukia Algeria ishiriki kwenye mpango wa kupambana na Makundi ya Kiislam yaliyopo Kaskazini mwa Mali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akizungumza na Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akizungumza na Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ameongeza shinikizo kwa Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele kusaidi juhudi za kupelekwa kwa Jeshi nchini Mali kukabiliana na Makundi ya Waislam wenye msimamo mkali yaliyopo Kaskazini mwa Taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Clinton ameitoa alipokutana na Rais Bouteflika na kumsihi akiwa jirani wa Mali anastahili kufanya kila linalowezekana katika kupata suluhu ya kudumu nchini humo na kudhibiti kile ambacho kinaendelea kushuhudiwa Kaskazini ambalo lipo chini ya makundi ya Kiislam.

Marekani imeelekeza nguvu zake nchini Algeria kutokana na Taifa hilo kuwa na nguvu za kijeshi na za kiitelijensia ambazo zimefanikisha mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakichangia ukosefu wa usalama Kaskazini mwa Afrika.

Clinton ameongeza kuwa nguvu hizo za serikali ya Algeria kijeshi zinaweza zikatumika vyema kabisa katika kukabiliana na Makundi ya Waislam ambayo yanapatikana Kaskazini mwa Mali na kuchangia hofu ya taifa hilo kugawanyika.

Afisa ambaye amesafiri la Waziri Clinton huko Algeria amesema wameona kuna umuhimu wa kuishirikisha kwa karibu zaidi nchi hiyo kutokana na kuwa jirani mkubwa zaidi wa Mali hivyo wanaweza kusaidia kwenye juhudi za kurejesha amani huko Bamako.

Waziri Clinton ameweka bayana licha ya kuiomba Algeria kushiriki kwenye mpango huo lakini wataendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaka jeshi litakalopelekwa Kaskazini mwa Mali.

Marekani kwa kushirikiana na Ufaransa ndiyo zimekuwa mstari wa mbele wa kuishawishi Algeria iwe sehemu ya mpango wa kupelekwa kwa kikosi cha kijeshi nchini Mali wakiamini uzoefu wao wa kukabiliana na ugaidi utawasaidia kutimiza malengo yao.

Tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC limetoa wito kwa ECOWAS kuendelea na maandili ya kupata Jeshi ambalo litaenda kupambana na Makundi ya Kiislam ambayo yanapatikana Kaskazini mwa Mali.