Misri

Wamisri waitisha maandamano kupinga mamlaka ya rais

Rais wa Misri Mohamed Morsi akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilary Clinton
Rais wa Misri Mohamed Morsi akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilary Clinton REUTERS/Egyptian Presidency/Handout

Wafuasi na wapinzani wa rais wa Misri Mohamed Morsi wameitisha maandamano makubwa leo Ijumaa baada ya kiongozi huyo kujipa madaraka makubwa ambayo wachambuzi wansema kuwa yanamfanya kuwa dikteta. 

Matangazo ya kibiashara

Safu ya vikundi huria na visivyo na mlengo, ikiwa ni pamoja na wanaharakati waliokuwa mstari wa mbele katika harakati zilizomwondosha madarakani kiongozi mkongwe wa taifa hilo Hosni Mubarak mapema mwaka jana, wamepanga kufanya maandamano katika bustani ya Tahrir jijini Cairo, eneo ambalo ni kitovu cha maandamano, kupinga hatua ya kiongozi huyo ambaye amebatizwa jina la farao mpya.

Wafuasi wa Morsi wakiongozwa na chama chenye nguvu cha Muslim Brotherhood wamekusanyika nje ya kasri ya rais Kaskazini mwa jiji la Cairo kuonesha kuunga mkono uamuzi wa rais huyo kujiongezea madaraka na kujiweka juu ya sheria za nchi hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa rais Morsi anatafakari kuhusu kuhutubia umma wa taifa la Misri baadye hii leo kwa lengo la kutetea uamuzi wake.
Siku ya Alhamisi, rais alidhoofisha uwezo wa mahakama ambayo imekuwa ikifikiria kuweka usawa katika jopo linalotawaliwa na chama hicho cha kiislam kwa kutengeneza katiba mpya, kwa kuwaondolea majaji haki na mamlaka ya kuhoji kuhusu maamuzi yake.