Hali bado tete Misri, Rais Morsi ashikilia msimamo wakati maandamano yakitikisa nchi
Maandamano makubwa ambayo yamewaleta pamoja maelfu ya wananchi wa Misri kutoka Vyama vya Upinzani yamelitikisa taifa hilo na kutishia utawala wa Rais Mohamed Morsi aliyetangaza kujiongezea madaraka.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda nchini Misri na kushuhudia wafuasi wa vyama vya upinzani wakionesha hasira zao kupinga hatua ya Rais Morsi kujiongezea madaraka na wamemtaka kuheshimu katiba ya nchi hiyo.
Wafuasi wa vyama hivyo wamepiga kambi katika Viunga vya Tahrir wakisema watapambana kwa nguvu zao zote kuhakikisha Rais Morsi hafanikiwi katika kile ambacho anataka kukifanya kwa sasa.
Mandamano hayo yamewakusanya pia wanasheria ambao wanasema sekta yao imedhalilishwa kutokana na Rais Morsi kuamua kuingilia na kujivika madaraka ambayo hayakubaliki na katiba.
Wafuasi hao wa Vyama vya Upinzani wameshambulia hata ofisi mbalimbali za Chama Cha muslim Brotherhood wakionesha kukerwa na siasa za chama hicho na wengine wamefikia hatua ya kutaka Rais Morsi akae kando.