Misri yahimizwa kukomesha mauaji yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo
Imechapishwa:
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton ametoa wito kwa serikali ya Misri kurejesha utulivu na kuhakikisha pande zote zinalinda demokrasia ili kusitisha mauaji yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo. Wito huo unakuja baada ya watu thelathini kuuawa na wengine zaidi ya mia tatu kujeruhiwa katika vurugu za kupinga hatua ya jana jumamosi ya mahakama nchini humo kuwahukumu kifo watu ishirini na moja ambao ni mashabiki na wanachama wa vilabu mbalimbali vya soka nchini humo.
Rungu la mahakama limewashukia watu hao baada ya kudaiwa kuhusika na vurugu za mwezi february mwaka jana zilizozuka katika mchuano wa soka kati ya klabu ya al-Masry na al-Ahly zote za nchini Misri na kusababisha vifo vya watu sabini na nne.
Dakika chache baada ya hukumu hiyo kutolewa kuliibuka vurugu kubwa ambapo raia wamekabiliana na polisi waliokuwa wakitumia mabomu ya machozi na risasi za mipira kuwatawanya ndugu wa waliohukumiwa.
Ghasia hizo zilizuka siku moja tu baada ya watu wengine tisa kuuawa wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji siku ya ijumaa katika maadhimisho ya miaka miwili tangu kuangushwa kwa utawala wa Hosni Mubarak huku wakimtaka Rais wa sasa Mohammed Morsi kujiuzulu.