JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-DRC

Waasi wa Seleka wavamia mji wa Mobaye-Banga nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Raia zaidi ya elfu 3 kutoka mji wa Mobaye-Banga nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wamevuka mpaka na kukimbilia upande wa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika jimbo la Ikweta wakiwakimbia waasi wa kundi la Seleka ambao wamevamia mji wao bila kutoa taarifa yoyote.

Matangazo ya kibiashara

Raia hao wamesema walishangaa kuona baadhi ya viongozi wao wakiwamo wakuu wa polisi na maofisa wa shirika la uhamiaji wakiondoka na familia zao kukimbilia upande wa DRC, jambo lililopelekea wananchi nao kuanza kuyahama makazi yao.

Jumapili hii mkuu wa Wilaya ya Ubangi nchini DRC amesema kuwa wakimbizi wanaendelea kuingia kwa wingi na wamekusanyika katika mji wa Mobayi-Mmbongo bila ya kupata msaada wowote.

Wakuu wa mashirika ya kibinadamu wanasema wamepata taarifa ya uwepo wa wakimbizi na sasa wanajaribu kuchukua tahadhari haraka iwezekanavyo.

Mamia kwa maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Afrika ya Kati walikimbilia DRC wakati wa mapigano kati ya jeshi la serikali ya Afrika ya kati na waasi wa Seleka mwishoni mwa mwaka jana.