Kenya-Uchaguzi 2013

Wagombea wa urais nchini Kenya kumenyana katika mdahalo wa pamoja usiku huu

Mamilioni ya wakenya usiku huu watashuhudia mdahalo wa wagombea urais nchini humo kupitia vyombo vya habari , wiki tatu kabla ya uchaguzi Mkuu kufanyika. 

Matangazo ya kibiashara

Huu utakuwa mjadahalo wa kwanza baina ya wagombea hao na pia kuwahi kufanyika katika histori ya kisiasa nchini humo ambapo wagombea hao watatumia fursa hiyo kujibu maswali na kunadi sera zao.

Miongoni wa wagombea hao watakaomenyana katika mdahalo huo ni pamoja na Waziri Mkuu Raila Odinga kutoka muungano wa CORD, Manaibu wake Uhuru Kenyatta kutoka muungano wa Jubilee na Musalia Mudavadi wa muungano wa Amani.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria Martha Karua wa Narc, Peter Kenneth kutoka muugano wa Eagle na Profesa James Ole Kiayapi kutoka chama cha RBK.

Mdahalo huu utawaleta pamoja wagombea hao kwa mara ya kwanza baada ya kushudiwa wakitofauatiana katika majukwaa ya kisiasa wakati wa kampeni za kuelekea Ikulu.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema huenda mdahalo huo usibadilishe chochote miongoni mwa wapiga kura nchini humo kwa kile wanachokisema wapiga kura wengi wameshafanya uamuzi wao wa ni nani watakamyechagua.

Duru ya pili ya mdahalo huo utafanyika tarehe 25 mwezi huu wa pili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu tarehe 4 mwezi ujao wa tatu.