SUDAN KUSINI

Watu zaidi ya 100 wauliwa katika jimbo la Joglei Sudan Kusini

Watu zaidi ya 100 wakiwemo wanawake na watoto wameuliwa katika jimbo la Joglei nchini Sudan Kusini baada ya kushambuliwa na waasi.

Matangazo ya kibiashara

Vifo hivyo vimethibitishwa na Gavana wa jimbo hilo Kuol Manyang Juuk na kusema kuwa wanajeshi 14 kutoka Sudan Kusini pia waliuawa katika shambulio hilo wakati wakiwasindikiza wafugaji.

Jimbo la Jonglei limekuwa likishuhudia hali ya ukosefu wa usalama kwa kipindi kirefu sasa huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa zaidi ya watu 2,600 waliuliwa kati ya mwezi January mwaka 2011 na September 2012 katika makabiliano yanayolezwa kuwa ya kikabila.

Walioshuhudia mashambulizi hayo wanasema kuwa wanashuku kundi la waasi linaloongozwa na David Yau Yau ndilo ambalo lilitekeleza mashambulizi hayo.

Kundi hilo la waasi linalotokea jamii ya Murle limekuwa likitekeleza mashambulizi mbalimbali baada ya kupoteza uchaguzi wa wabunge mwezi Aprili mwaka 2010.

Kwingineko, hali ya usalama kati ya Sudan na Sudan Kusini haijatengemaa baada ya viongozi wa mataifa hayo mawili kushindwa kufikia mwafaka wa kuimarisha usalama, na maswala ya kiuchumi uliotiwa saini mwezi Septemba mwaka uliopita.