MALI

Al-Qaeda inataka vita vya Jihad nchini Mali

Kundi la kigaidi la Al-Qaeda linaloendeleza shughuli zake katika mataifa ya kiarabu linataka vita vya Jihad kufanyika nchini Mali.

Matangazo ya kibiashara

Wito wa kundi hilo lenye makao yake nchini Yemen unakuja siku mbili baada ya kundi la Kiislamu la MUJAO kuanza kushambuliana na wanajeshi wa serikali ya Mali na Ufaransa katika mji wa Gao.

Kundi hilo la AQAP limeshtumu serikali ya Ufaransa kwa kutuma vikosi vyake vya kijeshi Kaskazini mwa Mali kupambana na makundi hayo ya Kiislamu kitendo ambacho wanasema ni kupiga vita Uislamu .

Aidha, AQAP limeongeza kuwa litaendelea kuwasaidia waasi hao kifedha kadiri ya uwezo wao ili kuwasaidia kuendeleza shughuli zao Kaskazini mwa nchi hiyo na kuhakikisha kuwa mfumo wa Sharia unatekelezwa Kaskazini mwa taifa hilo.

Serikali ya Ufaransa ilianza oparesheni yake dhidi ya waasi hao wa Kiislamu mwezi uliopita baada ya ombi la serikali ya Mali kutokana na waasi hao kuthibiti Kaskazini mwa taifa hilo kwa kipindi cha miezi 10.

Paris ilituma wanajeshi elfu 4,000 ambao wako ardhini na wengine wanatumia Helikopta kupambana na waasi hao, na imefaulu kuwaondoa katika miji ya Timbukutu, Kidal na Gao na wanajiandaa kuondoka nchini humo kuazia mwezi ujao wa tatu.

Ufaransa inataka wanajeshi 8,000 kutoka Muungano wa Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS kuanza kuchukua maeneo yaliyothibitiwa na vikosi vyake na baadaye kujumuishwa katika Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani.

Hata hivyo, Mali bado haijaonesha nia ya kuunga mkono kuwepo kwa Majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani na kusaidia kupambana na waasi hao wa kiislamu kwa mujibu wa Ofisa wa Umoja wa Mataifa.