Marekani yataka Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono upatikanaji wa amani DRC
Imechapishwa:
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani kuhusu maswala ya Afrika anayemaliza muda wake Johnnie Carson, anataka Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Umoja wa Mataifa uko katika harakati za kuwasilisha mapendekezo mapya kwa viongozi wa Kusini mwa Afrika katika harakati za kumaliza ukosefu wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa vikosi vya jeshi kutumwa .
Umoja wa Mataifa unapanga kutuma wanajeshi 2,500 kukabiliana na waasi Mashariki mwa DR Congo mpango ambao ulikataliwa na viongozi wa Afrika mwezi uliopita jijini Addis Ababa Ethiopia kwa kile walichokisema kuwa hawakushirikishwa.
Carson ametoa wito kwa DR Congo na mataifa jirani kutia saini mapendekezo hayo ya Umoja wa Mataifa haraka iwezekanavyo ili kumaliza hali ya wasiwasi Mashariki mwa DRC.
Mazungumzo ya kusaka amani kati ya waasi wa M 23 na wajumbe wa serikali ya DR Congo yanayoendelea jijini Kampala Uganda kwa mwezi wa tatu sasa bado hayajazaa matunda.
Mamilioni ya watu wameuawa kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita Mashariki mwa DRC kutokana na uwepo wa makundi ya waasi nchini humo na pia katika mataifa mengine ya Maziwa Makuu.
Ikiwa mpango wa Umoja wa Mataifa utaridhishwa na viongozi wa mataifa ya muungano wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC, majeshi ya Umoja wa Mataifa yatakwenda Mashariki mwa DR Congo kupambana na vikosi vya waasi.