Kenya-Uchaguzi 2013

Wagombea wa urais nchini Kenya wamenyana katika mdahalo wa kwanza kuelekea Uchaguzi Mkuu

Wagombea wanane wa urais nchini Kenya walikabiliana vikali katika mdahalo wa urais wa kwanza katika historia ya kisiasa nchi humo wiki tatu kabla ya uchaguzi Mkuu wa tarehe 4 mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Mamilioni ya Wakenya na raia wengine wa Afrika Mashariki na duniani walifuatilia mdahalo huo kupitia vituo mbalimbali vya habari huku wakizungumzia maswala ya afya, elimu, ukabila na suala la ICC linalomkabili Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta anayewania urais kupitia muungano wa Jubilee.

Kenyatta alisema kuwa licha ya kukabiliwa na kesi katika Mahakama ya ICC haitakuwa kikwazo kwake kuongoza nchi hiyo hata wakati kesi itakapokuwa inaendelea mwezi wa Aprili ikiwa atachaguliwa kama rais.

Waziri Mkuu Raila Odinga akizungumzia suala hilo alisema itakuwa vigumu kwa Uhuru Kenyatta kuongoza Kenya wakati akiwa kizimbani na hata kueleza kuwa haitawezekana Uhuru  kuiongoza Kenya kupitia mtandao wa Skype.

Hata hivyo, wagombea wote Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, Martha Karua , Paul Muite waliunga mkono kesi hiyo kurudishwa nyumbani huku wakilaumu bunge kusababisha kesi hiyo kupelekwa Hague.

Kuhusu ukabila, Waziri Mkuu Odinga wa muungano wa kisiasa wa Cord alisema hilo ni janga ambalo linaweza kufafananishwa kama maradhi ya saratani wito ambao pia uliungwa mkono na Naibu wake Uhuru Kenyatta huku kila mmoja akisema atahakikisha usambazaji wa rasilimali unafanyika kwa usawa ili kumaliza ukabila.

Odinga na Kenyatta ambao wanapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo walituhumiwa kuongoza jamii kubwa nchini humo suala ambalo lilielezwa kusababisha ukabila nchini humo na siasa za Kenya kuegemea kisiasa.

Profesa James Ole Kiyapi,  Katibu wa zamani wa kudumu katika wizara ya afya na elimu alidokeza kuwa  ikiwa atapata nafasi ya kuingia Ikulu atabadilisha mfumo wa elimu  na kujenga madarasa zaidi katika shule zote nchini humo pamoja na hospitali.

Wakenya wanasema wamefurahishwa na mdahalo  huo ambao umewawezesha kuwafahamu  wagombea hao vema na kuona namna walivyojitetea na kunadi sera zao.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema mdahalo huo huenda usibadilishe pakubwa uamuzi wa wakenya kuelekea uchaguzi huo lakini huenda ukashawishi wakenya ambao hawajaamua kuegemea upande upi kufanya uamuzi wao.

Mjadala mwingine utafanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari wiki moja  kabla ya uchaguzi Mkuu kufanyika tarehe 4 Mwezi wa tatu.