ZIMBABWE

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ajiuzulu

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe Jaji Mustaafu Simpson Mutambanengwe amejiuzulu wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba mpya mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Mutambanengwe aliyechukua uongozi wa tume hiyo mwaka 2010 miaka miwili baada ya uchaguzi uliokumbwa na visa vya wizi wa kura, na rais Robert Mugabe kutangazwa mshindi katika mazingira ya kutatanisha ameamua kuachia wadhifa huo kutokana na sababu za kiafya.

Waziri wa Sheria na Katiba nchini humo Patrick Chinamasa akithibitisha kujiuzulu huko, amesema tayari rais Robert Mugabe amekubali uamuzi wa kujiuzulu kwa Mutambanengwe.

Waziri huyo anasema kwa sasa mashauriano yanafanyika kati ya rais Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ili kumpata Mwenyekiti mpya wa tume hiyo ya uchaguzi.

Zimbabwe inatarajiwa kuandaa uchaguzi Mkuu na kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba mpya baadaye mwaka huu kumaliza malumbano katika serikali ya muungano lakini haijabainika ni lini uchaguzi huo utafanyika.

Tayari chama cha rais Mugabe cha ZANU PF na kile cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai cha MDC vimeafikiana kuhusu kufanyika kwa kura ya maoni kuamua mustakabali wa rasimu ya katiba mpya nchini humo.

Hata hivyo, chama cha MDC kinasema kinataka mabadiliko zaidi kuhusu utendajikazi wa vyombo vya habari nchini humo, idara ya usalama na tume ya uchaguzi nchini humo ili kuwezesha uchaguzi uwe huru na haki.

Aidha, Chama hicho cha Tsvangirai kimeendelea kudai kuwa Makamishena katika tume ya uchaguzi nchini humo wana idadi kubwa ya maafisa wa idara ya usalama wa kitaifa jambo ambalo wanasema ni sharti Makamishena wapya kuteuliwa.