Sudan Kusini inasema Sudan inasafirisha wanajeshi wake mpakani
Sudan Kusini inaituhumu Sudan kwa kuanza kutoa mafunzo na kuwasafarisha wanajeshi wake katika mpaka wake jambo ambalo Juba inahofia litakwamisha utekelezaji wa mkataba wa maelewano wa kuondoa wanajeshi katika mipaka ya mataifa hayo mawili.
Imechapishwa:
Mwafaka huo uliofikiwa mwezi Septemba mwaka jana baina ya mataifa haya mawili chini ya usuluhishi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia hadi sasa haujaanza kutekelezwa kutokana na mataifa hayo kulaumiana kuwa kila taifa linakwamisha mpango huo.
Kuondoka kwa wanajeshi wa mataifa hayo mawili katika mipaka yake kutawezesha Sudan Kusini kuanza kusafirisha mafuta yake kupitia Sudan baada ya biashara hiyo kukwama kutokana na tuhma za Juba kuwa inatozwa na Khartoum fedha nyingi wakati wa kusafirisha mafuta yake.
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusioni Majak D'Agoot amesema tayari serikali yake imewashajulisha mataifa jirani, Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hatua hiyo ya Sudan ambayo anasema ni kuingilia mipaka yake, tuhma ambazo Sudan haijazungumzia.
Wajumbe kutoka Sudan na Sudan Kusini wanatarajiwa kurejea jijini Addis Ababa Mwezi huu kujadili kukwama kwa mwafaka baina yao suala ambalo
wachambuzi wa siasa za Sudan wanasema huenda kikao hicho kisipate suluhu la kudumu kwa sababu ya kutoaminiana kwa viongozi wa mataifa hayo mawili.
Mwezi uliopita rais wa Sudan Omar Al Bashir na mwenzake wa Sudan Kusini Salva Kiir walikutana kujadili mwafaka huo na kushindwa kupata mwafaka.