UN-MALI

Umoja wa Mataifa waonya kutokea kwa machafuko Kaskazini mwa Mali

Umoja wa Mataifa unasema huenda kukatokea na machafuko zaidi  Kaskazini mwa nchini ya Mali baada ya shambulizi la kushtukiza mwisho wa juma lililopita lililotekelezwa na kundi la waaasi la MUJAO katika mji wa Gao dhidi ya wanajeshi wa taifa hilo na wale wa Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na maswala ya haki za binadamu Navi Pillay ameonya kuwa ikiwa mashambulizi hayo yataendelea na usalama kutoimarishwa vema huenda watu zaidi wakapoteza maisha yao.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 377,000 wamekimbia makwao Kasakzini mwa nchi hiyo kutokana na uwepo wa waasi hao wa Kiislamu ambao kwa sasa wamefurushwa na vikosi vya kijeshi kutoka Ufaransa.

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema serikali yake itasaidia kuwashinda waasi hao wa kiislamu wanaoshirikiana kwa karibu na kundi la kigaidi la Al- Qaeda.

Wakati uo huo,  kundi la kigaidi la Al-Qaeda linaloendeleza shughuli zake katika mataifa ya kiarabu linataka vita vya Jihad kufanyika nchini Mali.

Wito wa kundi hilo lenye makao yake nchini Yemen unakuja siku mbili baada ya kundi la Kiislamu la MUJAO kuanza kushambuliana na wanajeshi wa serikali ya Mali na Ufaransa katika mji wa Gao.

Kundi hilo la AQAP limeshtumu serikali ya Ufaransa kwa kutuma vikosi vyake vya kijeshi Kaskazini mwa Mali kupambana na makundi hayo ya Kiislamu kitendo ambacho wanasema ni kupiga vita Uislamu .