Mwanaharakati nchini Kenya afika Mahakamani kutaka kuzuiliwa kwa waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya na Marekani
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mwanaharati mmoja nchini Kenya amefika katika Mahakama Kuu jijini Nairobi kuitaka Mahakama hiyo kuizuia Tume ya Uchaguzi nchini humo kuwaruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka barani Ulaya na Marekani kushiriki katika uchaguzi wa tarehe 4 mwezi ujao nchini humo.
Mwanaharakati huyo Samson Owimba Ojiayo amesema amechukua hatua hiyo kwa kuituhumu Umoja wa Ulaya na Marekani kuegemea upande mmoja kuhusu ni nani wanayemuunga mkono katika uchaguzi huo.
Mahakama jijini Naiorbi imesema itasikiliza kesi hiyo siku ya Jumatatu juma lijalo kutokana na uharaka wa suala hilo linalohusu uchaguzi wa Kenya.
Mapema juma hili Waziri wa Mambo ya nje wa Kenya Profesa Sam Ongeri alikutana na Mabalozi kutoka Umoja wa Ulaya jijini Nairobi kueleza masikitiko ya serikali yake kwa madai kuwa wanatishia kuitenga Kenya ikiwa Uhuru Kenyatta anayeshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa tuhma za kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi Mkuu nchini humo mwaka 2007 atashinda katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umekanusha madai ya serikali ya Kenya kuwa utaiwekea vikwazo Kenya ikiwa Uhuru Kenyatta atachaguliwa kama rais na William Ruto kama naibu wake na badala yake kusema Umoja wa Ulaya unaounga mkono uchaguzi ulio huru na haki na wenye amani na hauegemei upande wowote.
Siku ya Alhamisi, Mahakama ya ICC itafanya kikao na washukiwa hao huku Uhuru Kenyatta na William wakitumia teknolojia ya video kusikiliza na kufuatilia mipangilio ya kesi yao itakavyokuwa kuanzia mwezi wa Aprili , huku aliyekuwa Mtumishi wa Umma Francis Muthaura na Mwandishi wa habari Joshua Arap Sang wakihudhuria kikao hicho huko Hague.
Siasa za Kenya zinaendelea kupamba moto wiki tatu kabla ya uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 4 mwezi wa tatu huku kura ya maoni kutoka shirika la IPSOS Synovate ikimpa uongozi Uhuru Kenyatta kwa alama 40 huku Raila Odinga akiwa wa pili kwa asilimia 33 kutokana na mdahalo wa mapema juma hili ya wagombea urais.
Mdahalo mwingine utafanyika tarehe 25 mwezi huu wiki moja kabla ya uchaguzi ambapo wagombea watazungumzia maswala ya ardhi na sera ya mambo ya nje ya Kenya pamoja na maswala mengine.
Wagombea wanane wanawania wadhifa huo huku ushindani mkubwa ukiwa kati ya Waziri Mkuu Raila Odinga wa muungano wa CORD na Naibu wake Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee.