Mwanariadha maarufu nchini Afrika Kusini Oscar Pistorius afikishwa Mahakamani
Viongozi wa Mashtaka katika Mahakama moja mjini Pretoria nchini Afrika Kusini wanasema kuwa kesi dhidi ya mwanariadha maarufu mwenye ulemavu Oscar Pistorius itakuwa ya mauaji ya kupanga.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26 anatuhumiwa kumuua kwa kumpiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp siku ya Alhamisi akiwa nyumbani kwake.
Pistorius ambaye amefikishwa Mahakamani siku ya Ijumaa na kusomewa mashtaka yanayomkabili, aliangua kilio mbele ya Jaji na kurudishwa kizuizini kusubiri kuanza kwa kesi yake siku ya Jumanne juma lijalo.
Imebainika kuwa mwanariadha huyo alimpiga risasi nne mpenzi wake kichwani na mikokoni kwa mujibu wa ripoti ya awali iliyotolewa na polisi nchini humo.
Siku ya Alhamisi, ilidaiwa kuwa Pistorius alitekeleza shambulizi hilo kwa kushuku kuwa aliyemshambulia alikuwa jambazi aliyekuwa amemvamia nyumbani kwake.
Ikiwa atapatikana na hatia atafungwa maisha jela.
Mwanaridha huyo mlemavu wa miguu yote miwili atakumbukwa sana kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 na kuweka historia katika michezo iliyomalizika ya Olimpiki jijini London nchini Uingereza mwaka uliopita.
Mwaka 2008 Pistorius alishinda kesi na kuruhusiwa na shirikisho la riadha duniani IAAF baada ya kumruhusu kushiriki katika michuano ya Olimpiki kwa walemavu huko Beijing.
Visa vya mauaji kwa kutumia bastola nchini Afrika Kusini vimekuwa vikiongezeka katika siku za hivi karibuni.