AFRIKA KUSINI

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kutoa hotuba kwa taifa

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma siku ya Alhamisi atatoa hotuba kwa taifa wakati wa ufunguzi wa bunge mjini Cape Town.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya rais Zuma inakuja wakati huu ambapo waekezaji nchini wakiwa na wasiwasi kutokana na migomo na maandamano makubwa  ambayo yamekuwa yakiendelea kushuhudiwa hasa katika sekta ya madini.

Kiongozi huyo pia anatarajiwa kutumia hotuba hiyo kuwaondolea waekezaji hao wasiwasi na kuwahakikishia raia wa taifa hilo  kuwa uchaguzi wa mwaka ujao utakuwa huru na haki.

Tayari rais Zuma amepata idhini ya chama chake cha ANC kugombea urais kupitia chama hicho tawala licha ya ukosoaji mkubwa kutoka kwa upinzani nchini humo unaosema serikali  imeshindwa kutekeleza sera walizoahidi wakati wa kampeni zilizopita.

Wananchi nchini humo pia wanatarajiwa kusikia kutoka kwa rais wao kuhusu mipango ya serikali  hiyo namna itakavyoshughulikia ukosefu wa ajira  hasa kwa vijana suala ambalo linasalia kuwa changamoto kubwa nchini humo.

Mwezi uliopita zaidi ya watu elfu 50 walipoteza kazi katika sekta mbalimbali nchini humo suala ambalo wachambuzi wa maswala ya uchumi wanasema linaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa serikali.