KENYA-ICC

Uhuru Kenyatta na Francis Muthaura waomba Majaji wa ICC kuahirisha kesi yao

Mgombea urais kupitia muungano wa Jubilee nchini Naibu Waziri Kenya Uhuru Kenyatta na aliyekuwa wakati mmoja Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini humo Francis Muthaura wote wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa tuhuma za kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini humo mwaka 2007 wanataka kesi dhidi yao iahirishwe kutoka mwezi wa Aprili.

Matangazo ya kibiashara

Mawakili wa washukiwa hao wamesema wanahitaji muda zaidi ili kuandaa utetezi wao kwa kile wanachokieleza kuwa Kiongozi wa Mashtaka amewasilisha ushahidi mpya dhidi ya wateja wao.

Wakili wa Uhuru Kenyatta Steve Kay amewaambia Majaji wa Mahakama ya ICC huko Hague kuwa mteja wao sasa anatuhumiwa na mashtaka mengine baada ya upande wa Mashtaka kumpoteza shahidi waliokuwa wanamtegemea aliyedai aliletwa katika Mahakama hiyo kusema uongo dhidi ya Kenyatta.

Naye wakili wa Muthaura Karim Khan amesema anahitaji muda zaidi kwa sababu upande wa Mashtaka haujamwasilishia ushahidi kama inavyohitajika kisheria ili kujiandaa ipasavyo na pia kuongeza kuwa asilimia 68 ya kesi dhidi ya mteja wake ni mpya.

Hata hivyo, Wakili anayewakilisha waathiriwa wa machafuko hayo amepinga ombi la Mawakili hao kwa kile alichokieleza kuwa waathiriwa hao wamechoka na wanataka haki ifanyike haraka iwezekanavyo.

Majaji wa Mahakama hiyo wakiongozwa na Kuniko Ozaki tayari wamepanga kuwa kesi hiyo itasikilizwa mwezi wa Aprili kipindi ambacho huenda kukawa na duru ya pili ya Uchaguzi wa urais nchini Kenya.

Uhuru Kenyatta ambaye hakufika katika Mahakama hiyo alikuwa anafutalia matukio hayo kupitia mkanda wa Video akiwa jijini Nairobi .

Ijumaa itakuwa ni fursa ya washukiwa wengine William Ruto na Mwandishi wa habari Joshua Arap Sang ambapo Mahakama hiyo itakuwa inatoa mwelekeo wa kesi yao itakavyokuwa mwezi wa nne mwaka huu.