Al-Shabab wadai kumyonga mwanajeshi wa Kenya
Wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia wanadai kuwa wamemnyonga mwanajeshi mmoja wa Kenya na kuonya kuwa itatekeleza mauaji zaidi ya mateka wengine watano raia wa Kenya wanaowazuia.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Taarifa kutoka kwa kundi hilo inasema ilitoa siku ya mwisho kuwa ya tarehe 14 mwezi wa Februari kwa serikali ya Kenya kuyaondoa majeshi yake nchini humo na kuwaachilia huru washukiwa wanaotuhumiwa kushirikiana na kundi hilo ili kusitisha mauaji hayo.
Mwezi uliopita, kundi hilo lilitoa kanda ya video ikionesha mateka wa Kenya wakiiomba serikali jijini Nairobi kuwasaidia ili kuepuka kuuliwa na wanamgambo hao kwa kipindi cha siku tatu ikiwa Kenya haingeridhia matakwa yao.
Tangu majeshi ya Kenya KDF yalipovamia Somalia mwaka 2011 kupambana na wanamgambo hao, kumekuwa kukitokea kwa mashambulizi ya Gruneti jijini Nairobi na Mombasa pamoja na miji iliyokaribu na Somalia.
Tayari majeshi ya Kenya yamefaulu kuthibiti maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na kundi la Al-Shabab na kufaulu ikiwemo ngome yao kuu ya Kismayo.
Katika hatua nyingine, afisaa wa juu wa serikali ya Somalia ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa hawataki jeshi la Umoja wa Afrika AMISOM kupewa jukumu la kupambana na wanamgambo hao majini.
Kenya ndio nchi ya pekee katika jeshi hilo la Umoja wa Afrika ambayo imetuma wanajeshi wake wa majini kupambana na wanamgambo hao na imetaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha bajeti ya Dola Milioni 10 kufanikisha oparesheni hiyo.
Naibu Waziri Mkuu wa Somalia na Waziri wa Mambo ya nje Fawzia Y. H. Adam kuwa taifa lake linahitaji jeshi la AMISOM kupambana na Al-Shabab ardhini wala sio katika bahari Hindi suala ambalo Kenya inasema haijafurahishwa na hatua hiyo ya Somalia.